Top-ads

Powered by Blogger.

WELCOME.... MESAC OPEN SCHOOL - MWENGE ......BE EDUCATED TO LIVE AS YOU WISH, MESAC OPEN SCHOOL - MWENGE FOR YOUR FUTURE.......WELCOME ...MESAC OPEN SCHOOL - MWENGE ......BE EDUCATED TO LIVE AS YOU WISH, MESAC OPEN SCHOOL - MWENGE FOR YOUR FUTURE......WELCOME... MESAC OPEN SCHOOL - MWENGE ......BE EDUCATED TO LIVE AS YOU WISH, MESAC OPEN SCHOOL - MWENGE FOR YOUR FUTURE......

MTIHANI WA KUJIPIMA KIDATO CHA TANO KISWAHILI – 1

By | Leave a Comment
MTIHANI WA KUJIPIMA
KIDATO CHA TANO
KISWAHILI – 1
121/1
MUDA. SAA 2:30                                                                                                           
MAELEKEZO:
1. Karatasi ina sehemu A, B na C.
2. Jibu kwa kuzingatia maelekezo ya kila sehemu  na kila swali
3. Andika majina yako kama yalivyosajiliwa.
4. Zingatia usafi wa kazi yako.
5. Swali lisilo na namba halitasahihishwa.


SEHEMU A(Alama 30 )
UFAHAMU
Jibu maswali yote sehemu hii.
1. Soma kwa makini kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu maswali yanayofuata.
Katika Kijiji cha Matare Wilaya ya Mugumu Serengeti, Bwana Wambura alikamatwa kwa kesi ya kusingiziwa na kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu. Hukumu hiyo ilimtesa sana kichwa chache, alitamani kila mtu anayemhisi kuwa ana makosa aingie katika moyo wake na kuupata ukweli. Alilia na umaskini wake, labda angepata wakili mzuri angeweza kumtetea, kumkosa wakili kukahalalisha kifungo hicho!! Alikwenda gerezani huku akiumia sana.

Aliyaanza maisha mapya kwa shida sana, akawa mnyonge kila mara na mwili ukapoteza afya kiujumla. Huko gerezani alifanikiwa kupata rafiki aliyekuwa na cheo au jukumu la uzikaji wa wafungwa hasa wale ambao hawakuwa na ndugu ama ambao ndugu zao huwa hawajitokezi pale gerezani. Mzikaji alijaribu sana kumtia moyo Wambura na kumwaminisha kuwa hiyo ilikuwa hatua tu ya maisha anapaswa kuizoea na siku moja ukweli utajulikana tu!

Bwana Wambura maneno ya mzikaji hayakumwingia kabisa alizidi kunyong’onyea. “Siwezi kuvumilia kukaa gerezani miaka mitatu…….kama unajali kilio change unisaidie nitoroke kwa namna yoyote ile ndugu yangu.” Wambura alimsihi mzikaji.

Siku moja mzikaji akamwambia Wambura kuwa msaada umepatikana. Lakini yataka moyo!! “Nipo tayari kwa lolote alimradi tu nitoke humu” Alijibu Wambura, “Msaada pekee wa kukutorosha humu ndani ni kwa njia ya jeneza………yaani mfungwa akifa mimi nakuunganisha naye kwenye jeneza……” Akashusha pumzi kisha akaendelea, “wewe ukisikia kengele ya msiba, njoo mara moja kwenye chumba cha maiti, utakuta tayari sanduku liko katikati ya chumba litakuwa halijafungwa, funua mfuniko kisha ingia ndani yake ulale pembeni ya maiti kwani sanduku huwa kubwa la kutosha kila aina ya maiti na hata miili miwili inaingia.” Kisha nitakuja na kulipigilia misumari. Baada ya muda tutalipakia kwenye gari kwenda kuzika nje ya gereza.

Tutakuzika huko lakini baada ya dakika 20 hadi 30 nitarudi kukufukua. Hautashindwa kupumua kwa dakika hizo, utatoka ukiwa huru. Japokuwa wazo lilikuwa zuri lakini lilimtisha sana Wambura. Hata hivyo akaona afadhali afanye hivyo kuliko kukaa gerezani miaka mitatu bila kosa.

Siku moja Wambura akasikia kengele ya msiba na mara moja akafanya kama alivyoelekezwa na mzikaji. Akaenda na kuingia chumba cha maiti. Kweli akakuta sanduku, akiwa na hofu kuu akaingia na kulala pembeni ya maiti iliyokuwemo. Mara akasikia mtu ameingia na kupigilia misumari sanduku. Muda mfupi baadaye sanduku likainuliwa na kuwekwa kwenye gari. Gari lilitoka nje ya gereza hadi makaburini, sanduku likashushwa na kuwekwa kaburini na kuanza kufukiwa. Wambura alijitahidi sana kuvumilia japo hofu ilizidi kutanda. Alimtegemea sana mzikaji na alianza kumwona mkombozi wa maisha yake. Kama alivyoambiwa akasubiri dakika kumi, ishirini…..zikapita kimya! Dakika thelathini kimya! Joto nalo likazidi kuongezeka akajiongezea kauli ya ujasiri, “Kama nilitakiwa kuishi gerezani miaka mitatu kivipi dakika kadhaa za hapa kaburini zinishinde.”

Kwakuwa alishakaa gerezani kwa muda kiasi akatamani kujua aliyekufa ni nani…… ni kweli aliogopa kuitazama maiti lakini aliona kama inatisha zaidi ikiwa imefunikwa vile kuliko ikiwa wazi. Akaifunua upande wa usoni, kwa kuwa kulikuwa na giza nene alikodoa sana macho kuitazama LA HAULA!! MACHO YAKAKUTANA NA SURA YA WAMZIKAJI, MZIKAJI ALIKUWA AMEKUFA NA KUZIKWA NA AHADI ZAKE ZA UKOMBOZI.

MASWALI:
(a) Pendekeza kichwa cha habari kifaacho kwa habari hiyo.
(b) Wambura alifungwa kwa kosa gani?
(c) Kwa mujibu wa habari ni msaada gani alioukosa Wambura kuhusu masuala ya kisheria?
(d) Mwandishi ana maana gani anaposema, “……..alilia na umaskini wake?”
(e) Kama habari hii itawekwa katika tamthiliya itakuwa aina gani ya tamthiliya?

2. Fupisha habari hiyo kwa maneno mia moja (100)

SEHEMU B (Alama 40)
SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA
Jibu maswali mawili (2) sehemu hii.
3. Sentensi zifuatazo zina makosa . Zirekebishe kwa kuzingatia matumizi sahihi ya
     lugha.
(a)   Dawa hizi hutumika kwa watu wengi.
(b)  Nimeunywa uji wote.
(c)   Kesho siji kwenu.
(d)  Juma anamiliki duka la madawa.
(e)   Leo Dude amewekwa rizevu.
(f)   Amepata wazifa mzuri kazini.
(g)  Jana nilivyofika hukuwapo.
(h)  Hatusomagi mara kwa mara.
(i)    Baba ameniletea matunda juzi.
(j)    Kwa nini hujaosha vyombo jana?

4. Onesha  kosa la kisarufi katika  sentensi  zifuatazo, kisha  uziandike  kwa
     usahihi ukizingatia mpangilio kama unavyoonekana.

(a)  Baba huwaga hapendi fujo.
Kosa ……………………………………
Sahihi……………………………………

(b) Wakati huu atakuwa aidha nyumbani au kazini.
Kosa ……………………………………
Sahihi…………………………………...




(c)  Katika ajali ya basi mkoani Mwanza, watu 36 waliuwawa palepale.
Kosa ………………………………….
Sahihi…………………………………

(d) Enyi ndugu zangu samahanini kwa makosa niliyowatendea.
Kosa ………………………………….
Sahihi……………………………………………

(e)  Takadiri anasambaza vitabu mashuleni.
                     Kosa ………………………………….
                     Sahihi…………………………………
5. (a) Nini maana ya mzizi wa neno?
    (b) Onesha mizizi ya maneno yafuatayo:-
(i)             Salisha
(ii)           Anakunywa
(iii)         Onyesha
(iv)         Onesha
SEHEMU C (Alama 30)
UTUNGAJI
Jibu swali la sita (6)
6. Andika insha ya maneno yasiyopungua mia tatu na hamsini  na yasiyozidi mia
     nne kuhusu utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.


KUPATA MITIHANI YA SHULE MBALIMBALI TEMBELEA 
www.mwalimuwakiswahili.co.tz

Newer Post Older Post Home

0 Maoni: